Utoto Mtakatifu

Utangulizi

Awali, Shirika la Mtoto Yesu lilikuwa ni sehemu tu ya Shirika la Uenezaji Injili au Uenezaji Imani. Lakini kadri lilivyoenea na kukomaa, lilipata hadhi ya kuwa Shirika kamili lenye kujitegemea kwa kiasi fulani.

Mnamo mwaka 1842, Paulina Jaricot, mwanzilishi wa Shirika la kueneza imani, alimweleza Askofu Forbin-Jonson wa Nancy (Ufaransa) maoni yake kwamba ingefaa kuanzisha chama cha pekee kwa ajili ya watoto Wakatoliki ili kuwajengea moyo wa kimisionari tangu udogo wao kwa kujali shida na mahitaji ya watoto wenzao katika nchi za misioni.

Historia

Askofu Forbin-Jonson alitambua mara moja umuhimu wa chama cha namna hiyo. Ndiyo chama hicho kikaundwa na kikaanza kuenea kwanza katika miji ya Ufaransa. Pole pole kilienea pia katika nchi nyingine, na hatimaye Baba Mtakatifu alikitambua, akakipokea na kukipatia hadhi ya kuwa Shirika la Kipapa na kuhimiza lienezwe kote katika Kanisa Katoliki.

Tangu miaka michache baada ya kumalizika kwa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikani, Maaskofu Katoliki nchini Tanzania waliamua kuwa shirika hilo lianzishwe pia hapa nchini kwetu.

Lengo na Maono

Wakati shirika hilo lilipoanzishwa huko Ufaransa, tatizo kubwa lililoonekana kuzikabili nchi za misioni lilikuwa ni idadi kubwa ya watoto, hasa katika nchi ya India, walioachwa yatima ama kwa kufiwa na wazazi au kwa kutupwa. Kwa hiyo, Paulina Jaricot alitamani kuwapatia wamisionari misaada ya sala na fedha ili kuwawezesha kuwapokea angalau baadhi ya watoto yatima, kuwapa makazi na chakula, na kuwalea katika imani Katoliki.

Uanachama

Shirika la Mtoto Yesu ni hasa kwa ajili ya watoto, lakini haliwahusu watoto pekee, bali hata watu wazima wanaweza kujihusisha nalo.

Masharti ya Kuwa Mwanachama

Masharti ya kuwa mwanashirika ni mawili rahisi:

  • Sala: Wanashirika wasali kila siku sala ya Salamu Maria na kuongeza maombi:
    “Bikira Maria Mtakatifu, utuombee sisi na watoto wote maskini na wenye shida popote ulimwenguni.”
  • Sadaka: Wanashirika wanahimizwa kutoa sadaka kusaidia watoto wenye mahitaji.

Utoto Mtakatifu

Fungu la Biblia

Marko 10:14 - "Yesu alipoona hayo, alikasirika, akawaambia, 'Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni wao.'"

Hitimisho

Utoto Mtakatifu ni mwito wa kuwaandaa watoto na waumini wote kuwa sehemu ya kazi ya kimisionari, kwa sala na msaada wa sadaka, ili kuwasaidia watoto wenye shida ulimwenguni.